Utaratibu wa kuhama Mtandao Bila kubadili Namba – Mobile Number Portability

Mwandishi Diana Benedict

Huduma ya Mobile Number Portability ina maana gani?

Huduma ya kuhamia mtandao mwingine bila kubadili namba ya simu ya kiganjani (MNP), ina maana kuwa mtumiaji anabaki na namba yake ya awali iwapo ataamua kuhamia mtandao mwingine wa simu za kiganjani nchini Tanzania. Kimsingi, ni huduma ambayo inakuwezesha kubakia na namba yako bila kujali unatumia mtandao gani. Hivyo, iwapo utabadilisha mtoa huduma wa simu za kiganjani hutakuwa na haja ya kusumbuka kuwataarifu watu wako wa karibu – marafiki, familia na wafanyakazi wenzako au washirika katika shughuli zako kwamba umebadilisha namba kwani inabakia ileile.

Courtesy of Google

Huduma ya MNP ina faida zipi?

Utaendelea kutumia namba yako ya awali unapohama kutoka mtoa huduma mmoja kwenda mwingine na hivyo kufurahia uhuru na huduma za mtoa huduma mpya.

Utapokea simu na meseji bila kujali ni mtandao upi umehamia na bila kuwa na haja ya kuwataarifu marafiki, familia na wafanyakazi  wenzako au washirika katika shughuli zako kwamba umebadilisha mtoa huduma wako.

Utaokoa fedha kwa kuwa hutakuwa na haja ya kununua laini mpya kwa kila mtoa huduma au kuwa na simu ya kiganjani zaidi ya moja.

Utaweza kuchagua mtoa huduma ambaye unaona anatoa huduma bora zaidi, anakidhi matarajio yako na ana ubunifu katika kutoa huduma.

Huduma hii ya kuhamia mtandao mwingine bila kubadili namba ya simu ya kiganjani   ilianzia Machi 2017 na Hakuna gharama za kuhama na namba yako. Hata hivyo, kabla ya kuhama itabidi ununue laini mpya ya simu ya kiganjani, yaani “SIM card” kutoka kwa mtoa huduma mpya.

Mobile Number Portability

UTARATIBU WA KUHAMA

 1. Nenda vituo vya mauzo au kwa wakala anayetambuliwa wa mtoa huduma unakotaka kuhamia na umueleze mhudumu kwamba ungependa kuhama na namba yako.
 2. Mhudumu atakutaka ujaze fomu maalum ya maombi (fomu moja).
 3. Sehemu ya Fomu ya maombi ya kuhama ni tamko rasmi kwamba unakubali kuwa utawajibika kwa madeni yoyote ambayo yanatokana na huduma ulizokuwa unapata kutoka kwa mtoa huduma wako wa awali kama yapo.
 4. Utatakiwa kutoa vitu vifuatavyo: –

a) Kitambulisho chenye picha yako – kinaweza kuwa Kitambulisho cha Taifa, Kadi ya Mpiga Kura, Leseni ya Udereva au pasipoti au kitambulisho chochote rasmi kinachotambulika.

b) Simu ya kiganjani inayofanya kazi yenye namba unayotaka kubaki nayo.

 1. Iwapo una salio katika akaunti ya pesa mtandao utashauriwa kutoa pesa kabla ya kuhama ili kuepuka usumbufu kama ilivyoelezwa kwenye masharti ya kuhama.
 1. Utatakiwa kutuma meseji yenye neno “HAMA” kwenda namba ‘15080’ ambayo ni namba maalum ya kuhama. Msaada utatolewa iwapo utahitajika ili kufanikisha hili.
 2. Utapokea meseji kukujulisha kwamba maombi yako yamepokelewa.
 3. Iwapo namba yako haikuzuiliwa au kusimamishwa kwa muda kutokana na kutokukamilisha malipo ya madeni ya mtoa huduma wako wa awali, maombi yako yatashughulikiwa na utajulishwa kwa meseji kuhusu maendeleo ya mchakato huu.
 4. Mtoa huduma wako mpya wa huduma za simu za kiganjaji atakupatia laini mpya.
 5. Ili kuzuia kupokea mihamala ya fedha mtandao wakati wa kuhama, huduma za kifedha zitasitishwa kwa muda mpaka namba ikapohamishwa kwa mtoa huduma mpya, ambapo utatumia huduma zake za fedha mtandao kama utajiunga na huduma zipo.
 6. Katika kipindi cha kuhama huduma za kupiga na kupokea simu na ujumbe mfupi zitaendelea kama kawaida.
 7. Katika hali ya kawaida uhamaji utakamilika haraka, mara nyingi siku hiyo hiyo au, iwapo utachelewa sana, ndani ya siku mbili za kazi baada ya kukamilisha utaratibu wa maombi. Wakati huo namba yako itakuwa imeshahamishwa kwa mtoa huduma wako mpya na laini yako ya awali haitatumika tena. Utatumiwa ujumbe mfupi kuwa uhamaji umekamika na ubadilishe laini.
 8. Ikifikia hapo, weka laini mpya uliyopewa na mtoa huduma wako mpya kwenye simu yako. Iwapo huna uhakika wa nini cha kufanya, unaweza kwenda kwa mtoa huduma wako mpya au wakala wake au kuwapigia simu na wataweza kukusaidia.
 9. Mchakato umekamilika.

 

Number Portability

MASHARTI YA KUHAMA

Mfumo  wa kuhamia mtandao mwingine bila kubadili namba ya simu ya kiganjani utatumiwa na wateja wote nchini wanaolipia huduma kwanza na wanaolipia huduma baada ya matumizi. Ili kuingia kwenye mfumo huu, simu ya mtumiaji lazima iwe inatumika, yaani haijafungiwa au kusimamishwa kwa muda.

Ili kutumia huduma hii, inabidi kuzingatia masharti yafuatayo:-

 1. Iwapo ni mtumiaji anayelipia kabla ya huduma, yaani Pre-Paid :-
 2. a) Hutaweza kuhama na namba ambayo imefungiwa au kusimamishiwa huduma;
 3. b) Hutaweza kuhama na salio lililopo na utatakiwa kutumia salio hilo kabla ya kuhama la sivyo salio lako litapotea;
 4. c) Hutaweza kuhama iwapo una mkopo kutoka kwa mtoa huduma wako hapa nchini kama vile chini ya mfumo wa M-pawa na NipigeTafu au mikopo mingine kwa njia ya muda wa maongezi, pesa mtandao na kadhalika;
 5. d) Hutaweza kuhama iwapo namba yako inahusishwa na uhalifu na imefungiwa.

 

 1. Iwapo unatumia huduma kwa utaratibu wa malipo baada ya huduma, yaani Post-Paid ; zingatia masharti yaliyotajwa hapo juu ya wateja wa “pre-paid “ na masharti mengine yafuatayo :-

 

 1. a) Itabidi ulipe madeni ya matumizi yako kabla ya kuhama;
 2. b) Itabidi ukamilishe masharti ya msingi ya mkataba na mtoa huduma wako wa sasa na kutimiza masharti ya malipo kila mwezi kwa mujibu wa mkataba kabla ya kuhama;
 3. c) Utaendelea kupokea ankara za matumizi hadi namba itakapohamishiwa kwa mtoa huduma mpya. Utapokea ankara ya mwisho hadi siku 60 baada ya kuhamisha namba yako; kisha utapewa mpaka siku 30 za kulipa ankara hizo, vinginevyo utakuwa katika hatari ya uhamaji wako utasitishwa au namba yako kufungiwa.

 

ZINGATIA YAFUATAYO:

Hakuna gharama za kuhama na namba yako isipokuwa. Hata hivyo, kabla ya kuhama itabidi ununue laini mpya ya simu ya kiganjani, yaani “SIM card” kutoka kwa mtoa huduma mpya.

Wateja wote wanaotaka kuhama na namba zao na ambao wana salio katika akaunti ya pesa mtandao ni lazima walitoe salio hilo kabla ya kuhama vinginevyo salio litabaki bila mwenyewe na itabidi wafuate mchakato mrefu ili kuweza kupata pesa zao ambazo wakati wote zitakuwa salama hadi watakapokamilisha mchakato huo.

Tufuatilie @MtaawaSaba ili usipitwe na Habari, Uchambuzi naMakala mbali mbali ya mitanadoni na ya kiteknolojia kwenye Facebook, Twitter, Instagram, Google+ na Youtube, Pia usisite kutoa maoni yako hapo chini au tuandikie barua pepe kwa mhariri@mtaawasaba.com

 

Mwandishi Diana Benedict Mwandishi
Mitandao ya Kijamii
Diana Benedict. Digital Creator | IT Specialist | Graphics Designer | Web Designer | Web SEO | Contents Management | UI/UX Designer and Social Media Management.
1 Comment

Trending on Mtaawasaba

Receive Mtaawasaba notifications Click ‘Receive,’ then ‘Allow’ when prompted. Dismiss Receive