TTCL kutumia mabilioni kusambaza huduma ya internet majumbani

Mwandishi Alexander Nkwabi
Leo Jumanne Februari 27, 2018 Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL), bwana Waziri Kindamba ameeleza kuwa TTCL inatarajia kutumia Sh44.7 bilioni kusambaza intaneti ya kasi kubwa hadi majumbani kupitia huduma mpya iitwayo Fiber Connect Bundle, ambapo mteja atapata intaneti ya kasi isiyo na ukomo kwa gharama ya kuanzia Shilingi za kitanzania 100,000 hadi Shilingi 200,000 kwa mwezi.

Pia , Mteja atapata huduma za wireless service (WiFi) katika nyumba yake ambapo vifaa vyote vinavyotumia Teknolojia ya Intaneti vitaunganishwa na kuweza kutumia huduma hii. Mfano wa vifaa husika ni Smart Tv, Tablets, Laptops na kadhalika

Mwisho, Mteja atapatiwa vifaa  vyote bure pamoja na uhakika wa huduma za baada (After Sells Services) endapo itahitajika.

Mradi huu unatarajia kufikia nyumba takribani 500 maeneo ya Mikocheni na 500 zingine maeneo ya Mbezi Beach kwa jiji la Dar es Salaam, akaongeza kuwa sio Dar es Salaam pekee watakaofaidika na mpango huu bali nyumba zipatazo 200 mkoani Dodoma zilizo eneo la Medeli pia zitafaidika kabla huduma hii kusambazwa nchi nzima siku za usoni.

Akizungumza, Mkuu wa ufundi wa TTCL, Cecil Francis amesema mradi huu utagharimu kati ya dola za kimarekani milioni 15 mpaka 20 ambazo ni zaidi ya shilingi za kitanzania bilioni 33 mpaka 44 kwa awamu ya kwanza pekee. Tayari mradi huu ushaanza utekelezwaji tangu mwezi wapili mwaka huu.

Kwa sasa mradi upo kwenye majaribio ambao utachukua takribani miezi mitatu kabla huduma hazijaanza kutolewa katika majiji yote ya Tanzania Bara pamoja na Unguja katika awamu ya kwanza.

Akizungumzia  mwelekeo wa utendaji wa Shirika bwana Waziri Kindamba  amesema unaonesha ukuaji mzuri licha ya changamoto zilizopo. Mapato yameendelea kuongezeka na hasara kupungua kwa kiasi kikubwa, jambo linalotupa uhakika wa kutimiza ahadi yetu ya kutoa gawio Serikalini katika mwaka huu wa fedha 2017/2018.

TTCL itaendelea kuweka mkazo katika kuboresha eneo la Huduma kwa Wateja kwa kutoa huduma bora kwa gharama nafuu, kuongeza Wateja wapya, kusambaza huduma za 4G LTE katika Makao Makuu ya Mikoa yote Nchini ifikapo Juni 2018.

Aidha, tutaendelea kuongeza uwekezaji katika Teknolojia na Miundo mbinu yetu kote nchini, kuboresha mazingira ya kazi kwa Wafanyakazi na Vitendea kazi, kukusanya Madeni ya Shirika, kuongeza Wateja na ufanisi katika huduma za fedha Mtandao (TTCL PESA) na kuongeza ufanisi katika Miundombinu ya Kimkakati ya Serikali inayosimamiwa na kuendeshwa na Shirika la Mawasiliano Tanzania na hapa ninazungumzia Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano (NICTBB) na Kituo Mahiri cha kuhifadhia Kumbukumbu(National Data Centre).

 

Mwandishi Alexander Nkwabi Mhariri
Mitandao ya Kijamii
Alex ni mhariri mwandamizi hapa Mtaawasaba.com, kwa kipindi kirefu amekuwa akivutiwa na mfumo endeshi wa Android na michezo ya kompyuta. Alex akiwa haandiki hapa Mtaawasaba basi hupendelea kupiga picha, kusafiri na kusoma vitabu.
Maoni yako

Trending on Mtaawasaba

Receive Mtaawasaba notifications Click ‘Receive,’ then ‘Allow’ when prompted. Dismiss Receive